Wa Daima

Kweli u wewe mkongwe lakini hu dhaifu
Umejengwa kwa mawe, kwa chokaa na udongo
Umesimama imara, kwa dhamira na weledi
Mbele ya Bahari ya Hindi
Jua linakubariki
Mvua yakunawirisha

Waishuhudia miongo ipitavyo ikipishana
Pa mchoo paja vuli, pa kaskazi paja masika
Sekunde, dakika, saa, masiku, wiki, myezi na myaka
Shuhuda wa wajao kwa madau
Washukao kwa mabedeli
Waingiao kwa meli
Wangiao kwa vishindo, kedi, bezo na dharau
Na wajao kwa adabu, hishima na sitara zao
Bendera zikipepea, zikizeeka, zikichanika
Milingoti ikiwekwa na kuondolewa ama kuanguka
Wewe ulikuwepo
Bado upo
Na utakuwepo
Sababu japo u mkongwe
Daima wewe shujaa madhubuti
Wewe ndiye alama na sauti
Ya nchi hii ya Mwana wa Mwana
Taifa la Mwinyi Mkuu
Dola ya Mkamandume
Daima milele
Jana, leo na kesho

Mohammed K. Ghassani
21 Disemba 2015
Bonn